Description
Germany, Berlin
Ambassador
Congo (DR), Kinshasa
Ambassador
France, Paris
Ambassador
Congo (DR), Kinshasa
Ambassador
Burundi, Bujumbura
Ambassador
Balozi Andrew Kajungu Tibandebage alizaliwa mwaka wa 1921 katika kijiji cha Kasheshe Karagwe na kubatizwa kwenye Kanisa la Katoliki mwaka 1932. Alijiunga na Shule ya Msingi Bugene mnamo mwaka 1933 na mwaka uliofuatia alihamia shule ya Kajunguti – Rubya – Bukoba.
Elimu ya sekondari aliipata kwenye shule ya St Mary’s Tabora kati ya mwaka 1939 na 1941. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere – Uganda mnamo mwaka 1942.
Baada ya masomo yake, alifundisha kwenye shule yake ya St Mary’s Tabora. Akiwa mwalimu wa Kiingereza na Hisabati. Mwaka 1955 aliteuliwa kuwa mkuu wa Shule ya Kati ya Bugene Karagwe. Mwaka 1956 alihamishiwa sekondari ya Mtakatifu Thomas (Ihungo) Bukoba, kufundisha Kiingereza na kuwa mkuu wa Idara ya Hisabati.
Kati ya mwaka 1956 na 1957 alikuwa mhadhiri mshiriki katika Chuo Kikuu cha London. Aliporudi Tanganyika, aliendelea kufundisha Ihungo – Bukoba mpaka 1961 alipojiunga na utumishi wa umma serikalini.
Agosti 1961 alirudi London, Uingereza Kuhudhuria semina ya utumishi wa kidiplomasia. Na Septemba 1961 alifanya kazi katika Ubalozi wa Uingereza huko Ankra, Uturuki. Januari 1962 alifanya kazi katika Ubalozi wa Tanganyika huko London, Uingereza.
Ni mtu wa kwanza kufungua ubalozi wa Tanganyika nchini Ujerumani mnamo mwaka 1962. Februari 1963 aliteuliwa kuwa balozi wa kwanza wa Tanganyika nchini Ujerumani.
Balozi Tibandebage alikuwa pia mtu wa kwanza kufungua ubalozi wa Tanganyika kule Congo-Kinshasa na kuwa balozi kule hadi mwaka 1967 aliporudishwa nyumbani kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Utalii. Mwaka 1968 aliteuliwa tena kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, na mwaka 1970 alirudishwa tena nyumbani kuwa Msaidizi wa Rais (Mambo ya Nje). Mwaka 1972 alirudishwa Kinshasa kuwa Balozi wa Tanzania kwa nchi za Congo, Rwanda na Burundi. Desemba 21, 1975 aliacha kufanya kazi za kidiplomasia na Mei 31, 1976 akastaafu utumishi wa umma.
Aliporudi nyumbani kwao Karagwe aliendelea kushirikiana na wananchi kuiendeleza wilaya yao. Kazi hizi alizifanya kwa kujitolea bila kutafuta namna yoyote ile ya kujitajirisha. Aliwasaidia vijana wengi kwenda shule bila kujali uhusiano wa karibu.
Julai 1976 aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya uanzishwaji wa Shule ya Sekondari Karagwe. Leo hii, sekondari hiyo ni kati ya shule bora kwenye mkoa wa Kagera. Shule hiyo ilipofunguliwa mwaka 1977, Balozi Tibandebage ndiye alikuwa mwalimu mkuu wa kwanza. Baadaye aliteuliwa kuwa meneja wa shule hiyo na baadaye kabisa mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo. Kwa vile alikuwa na moyo wa kujitolea, Juni 1977 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Karagwe (KARADECO).
Mwaka 1984 Balozi Tibandebage aliteuliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe ambayo alitumikia nafasi hiyo kwa muhula mmoja; wakati huo huo aliteuliwa pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka ya Leseni za Usafirishaji, nafasi aliyoitumikia kwa kipindi cha miaka minne.