Description
Congo (DR), Kinshasa
Ambassador
USSR, Moscow
Ambassador
Isaac Abraham Sepetu alizaliwa oktoba 15, Mwaka 1943 huko Tabora, Tanganyika, lakini inatajwa kwamba wazazi wake waliamisha makazi yao kutoka tabora na kuamia kuishi visiwani Zanzibar, ambako hasa ndiko alipokulia na kusoma elimu ya msingi na sekondari , hii ilikuwa wakati Zanzibar ikiwa bado chini ya utawala wa kisultani. Kwahivyo kutokana na tamaduni na sheria za uraia wa Zanzibar, Isaac Sepetu akajikuta ni Mzanzibar ukizingatia pia uhuru wa nchi ya Zanzibar ulimkuta akiwa mkazi wa huko.
Balozi Isaac Abraham Sepetu alisoma elimu ya msingi na sekondari katika shule ya Mtakatifu Yusuf (St. Joseph school) moja ya shule maarufu sana wakati huo, kwasasa ikijulikana kama "Skuli ya Tumekuja" iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja hii ilikuwa kati ya mwaka 1952 - 1963. Baada ya kutoka St. Joseph school, Isaac sepetu alikwenda moja kwa moja Berlin Nchini Ujerumani, kujiunga na chuo kikuu cha Karl Max, (Karl Marx university) sasa kikiitwa Leipzig University, Ujerumani ( Siku hizo ikifahamika kama Ujerumani mashariki), hii ilikuwa kati ya mwaka 1964 -1970 ambako alisomea fani mbali mbali ikiwemo Uandishi wa Habari, Uhusiano wa kimataifa na baadaye kuhitimu shahada katika siasa za Uchumi (degree in Political Economy).
Balozi Isaac Abraham Sepetu ni moja kati ya wasomi mahiri na bingwa wa kuzungumza kwa ufasaha lugha kubwa tatu adhimu za kimataifa, kikiwemo kiswahili, kiingereza na kijerumani. Sifa zingine za kipekee alizokuwa nazo ni pamoja na utulivu wa kiakili, mtu asiye na papara, mwingi wa hekima, busara na maarifa na hakika sifa hizi ndizo hasa zilizomsaidia sana kufanikiwa katika maisha kama mtumishi wa umma, Mwanasiasa na baba wa familia ya Mke na watoto wanne (wakike) warembo akiwemo Bintie Wema Abraham Sepetu aliyepata kuwa mlimbwende wa Taifa mwaka 2006.
Isaac Abraham Sepetu alianza utumishi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 1970's Mara tu baada ya kurudi kutoka masomoni huko Ujerumani, ambapo alishika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadae katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius kambarage Nyerere.
Akiwa Zanzibar mwaka 1971 alifanya kazi katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama Mkuu wa Bizanje Msaidizi baadae akawa katibu mkuu wizara ya nchi, ofisi ya Rais wa Zanzibar, (Ikulu). Duru zinataja Kuwa alifanya kazi hizi za awali vizuri sana, tena kwa weredi mkubwa kutokana na uwezo wake kielimu, busara na maarifa aliyoyapata nchini Ujerumani Mashariki, nchi iliyokuwa ikiunga mkono sera za Ujamaa wakati huo, hakika sifa za utendaji kazi wa Balozi Isaac Sepetu zilimvutia sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere hata naye akamvuta katika serikali ya Muungano.
Kutokana na rekodi nzuri za utendaji kazi katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mwaka 1972, Rais Julius Nyerere akamteua Isaac Sepetu kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wadhifa aliodumu nao kwa miaka mitano (1972 -1977); Waziri wa Habari na Utangazaji kwa miaka miwili (1977 -1979); Waziri wa utalii na Maliasili kwa miaka mitatu (1979 -1982). Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Moscow kwa miaka saba (1982 - 1989) na Balozi wa Tanzania nchini Zaire sasa ikiitwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo (DRC) kwa mwaka mmoja (1989 -1990).
Mwaka 1990 Isaac Sepetu alirudi katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar pale alipoteuliwa na Rais Dkt. Salmin Amour (Komando) kuwa Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Mipango) nafasi hii aliishikiria hadi mwaka 2000, akiwa Waziri wa Nchi alikuwa pia Mshauri wa Rais wa Zanzibar katika masuala ya ushirikiano wa Kimataifa, Kutokana na heshima aliyojijengea katika siasa za Zanzibar, Isaac Sepetu alichaguliwa kuwa katibu wa kamati ya pamoja ya maridhiano, Zanzibar (IPC) kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wanachi (CUF). Kuanzia 2001 hadi 2005 Balozi Sepetu alikuwa mbuge katika Bunge la Afrika Mashariki, yaani "The East African Legislative Assembly" (EALA).
Balozi Isaac Sepetu anatajwa kama mmoja kati ya waasisi wa mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar wakati juhudi hizo zilipoanza kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa bara na visiwani mwaka 1995, tunaweza kusema kuwa hata matokea ya Maridhiano ya kisiasa Zanzibar ya mwaka 2008/2010 ambayo yalizaa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ni matokeo ya kazi ama jitihada za awali za Balozi Isaac Abraham Sepetu na wenzake akiwemo Chifu Emeka.
Balozi Isaac Abraham Sepetu pia amekuwa mtu muhimu sana katika Chama cha Mapinduzi tangu kuasisiwa kwake, hakika amekuwa kiunganishi kizuri na mmoja kati ya wanasiasa wachache waliofanikisha kuunganisha vyama viwili vya ukombozi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaani ASP cha Zanzibar na TANU cha Tanganyika mnamo mwaka 1977 kilipozaliwa Chama hichi tawala cha sasa "Chama cha mapinduzi" (CCM) yaani siku ile ya tarehe 5 Februari 1977. Isaac Sepetu amekuwa mjumbe wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (akitokea Zanzibar) kwa miaka 28. (1977 -2005)
Balozi Isaac Abraham Sepetu alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA). Wadhifa alioteuliwa kuendelea nao kwa mara nyingine na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dk. Ali Mohamed Shein, uteuzi uliotangazwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, tarehe 27 Machi, 2013.